

17 February 2025, 2:49 pm
“Wananchi wengi wanaogopa kujitambulisha kwa balozi sababu ya kuombwa elfu tano jambo ambalo halikubaliki katika mtaa wangu” – Mwenyekiti
Na: Kale Chongela – Geita
Serikali ya mtaa wa Mwatulole kata ya Buhalahala halmashauri ya manispaa ya Geita imewataka mabalozi wa mashina katika mtaa huo kutowatoza wananchi shilingi 5000 kama kiingilio kwenye mtaa huo.
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mwatulole Edward Msalaba akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 17, 2025 katika ukanda wa Samandito ambapo amesema changamoto ya baadhi ya wananchi kushindwa kwenda kujitambulisha kwa mabalozi ni kutokana na baadhi ya mabalozi kuwaomba fedha wananchi.
Kwa upande wake Balozi wa Shina 6, Benjamin Philibert amekanusha taarifa hizo kwenye mkutano wa hadhara kuwa yeye hajawahi kumtoza mwananchi kiasi chochote cha fedha kama sehemu ya kiingilio.
Baadhi ya wananchi walioshiriki Mkutano huo wa hadhara uliokutanisha wananchi kutoka katika Balozi 3 shina 02,shina 03 na shina 06 wamesema endapo kila balozi atasimamia majukumu yake itampa wepesi mwananchi kwenda kujitambulisha kwa balozi pindi anapohamia katika eneo lake.