

30 January 2025, 3:43 pm
“Ikifika muda kila mtu anajiuliza kwani nini chanzo cha haya yote, inabidi tumtumaini Mungu, kwani yeye ndiye mpangaji wa kila jambo” – Askofu Kanisa Katoliki Geita
Na: Mrisho Sadick – Geita
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko leo Januari 30, 2025 amewaongoza wakazi wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita kuaaga miili ya wanafunzi saba wa shule ya sekondari Businda waliofariki kwa ajali ya radi Januari 27 mwaka huu majira ya saa nane mchana baada ya mvua kubwa kunyesha.
Akizungumza na wananchi hao Dkt. Biteko ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao huku Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela akiwafaraji kwa kuwakumbusha kumtegemea Mungu katika kila jambo.
Mkuu wa shule ya sekondari Businda Bi. Theodora Mushi amesema wakati wa tukio la wanafunzi saba kufariki kwa kupigwa na radi wanafunzi wanne walifariki papo hapo na wengine watatu wakati wakipatiwa matibabu huku Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskas Muragili akieleza tukio hilo lilitokea saa nane mchana Januari 27, 2025.
Askof wa kanisa katoliki Jimbo la Geita Flavian Kasala na Shekhe wa wilaya ya Bukombe Ally Jumapili wameitaka Jamii kuwa na uvumilivu wakati wa matukio kama hayo kwakuwa ni mipango ya Mungu.