Miili 7 ya wanafunzi waliofariki kwa radi Geita kuagwa Januari 30
29 January 2025, 1:08 pm
Mvua iliyoambatana na radi iliyonyesha Januari 27, 2025 ilipelekea athari ikiwemo vifo pamoja na majeruhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe mkoani Geita.
Na: Mrisho Sadick – Geita
Miili ya wanafunzi saba waliofariki kwa ajali ya radi Januari 27,2025 katika shule ya sekondari Businda mkoani Geita kuagwa kesho alhamis Januari 30, 2025.
Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili amesema tayari wamewasiliana na familia za marehemu na kukubaliana miili ya wanafunzi hao kupewa heshima ya mwisho katika viwanja vya shule hiyo.
Mhe. Muragili amewataja waliofariki katika ajali hiyo Erick Bugalama (18) kidato cha tatu , Erick Akonai (18) kidato cha tatu , Nicas Tompoli (17) kidato cha tatu na Peter Nkinga (18) kidato cha tatu.
Wengine ni Gabriel Makoye (17) kidato cha 3 , Asteria Mkina (16) kidato cha tatu na Doto Masasi (17) kidato cha tatu.