

27 January 2025, 1:30 pm
Matukio ya waendesha pikipiki kujeruhiwa na kuporwa vifaa vyao vya kazi yanaendelea kuzua sintofahamu na swali likiwa nani kutegua kitendawili hicho.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa 20 hadi 25 ambaye ni dereva pikipiki maarufu kama boda boda mkazi wa kata ya Nyarugusu Halmashauri ya wilaya ya Geita amekutwa ameuawa na kuporwa pikipiki katika eneo la njia panda ya kutoka Nyarugusu kuelekea Geita mjini.
Wakizungumzia tukio hilo boda boda wenzake kutoka egesho la mawamelu kata ya Nyarugusu wamesema kijana huyo alipigiwa simu na mteja wake majira ya saa nne usiku kuwa anataka ampeleke Geita mjini na wakaelewana atampatia kiasi cha shilingi elfu thelathini (30,000) kwenda na kurudi ndipo alipoondoka katika egesho hilo na asubuhi wakapigiwa simu kuwa mwenzao amekutwa amefari huku mwili wake ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali.
Aidha Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kwaajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya halmashauri ya mji Geita huku boda boda wa nyarugusu zaidi ya 200 wakiusindikiza mwili wa kijana mwenzao kutoka eneo la tukio mpaka hospitalini huku wakiliomba jeshi la polisi kutafuta njia ya kukomesha vitendo vya utekaji na uporaji wa pikipiki wanavyofanyiwa boda boda katika mkoa wa Geita.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya mji Geita Dkt. Thomas Mafuru amekiri kupokea mwili wa kijana huyo ambapo ulikuwa na majeraha na kwa sasa umehifadhiwa kwaajili ya taratibu nyingine za kipolisi kuendelea.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Geita bado zinaendelea.