Mnyama Kiboko aliyesumbua kwa miaka 5 auawa Geita
23 January 2025, 4:21 pm
“Tunaishukuru serikali kwa kuweza kumuua mnyama huyu maana ilikuwa ni changamoto kubwa tukiishi kwa uoga”- mwananchi Itale
Na: Edga Rwenduru – Geita
Mnyama Kiboko aliyekuwa anaua mifugo na kuharibu mazao ya wananchi wa kijiji cha Itale kata ya Katoma halmashauri ya wilaya ya Geita ameuawa na Askari wa mamlaka ya usimamizi wa wanayamapori Tanzania TAWA usiku wa kuamkia Januari 22 mwaka huu.
Wananchi wa kijiji hicho wametoa shukrani kwa mamlaka ya wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kuchukua uamuzi wa kumuua kiboko huyo kwani wakazi wa kijiji hicho walikuwa wanaishi kwa hofu kubwa.
Josephat Komanya ni diwani wa kata ya Katoma amesema kuwa wakazi wa kijiji hicho sasa wamepata amani kwani mnyama huyo aliua ng’ombe watatu na kuharibu mazao huku akiiomba serikali na TAWA wadhibiti pia Mamba ambao ni tishio kwa maisha ya wakazi hao.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa Kamanda wa TAWA kanda ya ziwa Afisa wanyamapori msaidizi daraja la pili Sefu Marambo amesema hatua hiyo imekuja kufuatia barua waliyoipokea kutoka halmashauri ya wilaya ya Geita ikiwataka kumdhibiti Mnyama huyo.