Mbwa wanne wavamia mbuzi wawili na kuwaua Msufini
21 January 2025, 10:53 am
Wafugaji katika mtaa wa Msufini, Msalala road wahimizwa kuzingatia sheria ili kuondoa changamoto ya kupoteza mifugo yao kwenye mazingira mbalimbali.
Na: Amon Mwakalobo – Geita
Mwanaume mmoja kwa jina Mfaume Felix mkazi wa Msufini mtaa wa Msalala road manispaa ya Geita amemlalamikia jirani yake ambaye hajatambulika jina lake kwa kufungulia mbwa wake wanne bandani ambao walivamia mbuzi wake wawili wakiwajeruhi hadi kuwaua.
Akiongea na Storm FM Mfaume amesema tukio hilo limetokea siku ya Jumapili Januari 19, 2025 saa saba mchana wakati mvua ikinyesha ambapo alikuwa amewafunga nje wakila majani na baada ya mvua kukata alikuta mbuzi wake wamekufa huku baadhi ya majirani wakimwambia wameona mbwa wa jirani yake wakiwashambulia.
Mke wa Mfaume Alex aitwaye Khadija Abdallah amewasihi wafugaji wa mbwa kuwalinda ili kuondoa changamoto ambazo zinapelekea hasara kwa baadhi ya watu.
Baadhi ya wananchi wakizungumza kwa nyakati tofauti wamewashauri wafugaji kuzingatia maeneo ya ufugaji kwani maeneo ya mijini zinafanyika shughuli mbalimbali.
Kwa upande wa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Sostenes Kalist amekiri kupokea kesi hiyo lakini ameshindwa kuitolea maamuzi kwani hapakuwa na uthibitisho kama mbwa waliofanya tukio ni wa nani, lakini amewataka wananchi wanaofuga mifugi hasa mbwa kuhakikisha wanawafungia bandani kwani ndio utaratibu maana wanaweza hata kudhuru binadamu.