Atupiwa vitu nje kwa kushindwa kulipa kodi miezi 8
16 January 2025, 11:31 am
Wananchi wanakumbushwa kuzingatia suala la mikataba baina yao na wenye nyumba ili kuondoa migongano na migogoro baina yao.
Na: Kale Chongela – Geita
Mariasalome Stanslaus mkazi wa mtaa wa Msalala road kata ya Kalangalala halmashauri ya manispaa ya Geita amelalamikia kitendo cha kutupiwa vitu vyake nje na mwenye nyumba kwa kile kinachodaiwa kuchelewa na kushindwa kulipa kodi.
Akizungumza na Storm Fm Januari 15, 2025 Bi. Mariasalome amesema amekuwa mpangaji katika nyumba hiyo tangu mwaka 2021 na kwamba kitendo kilichofanyika dhidi yake si cha kiungwana.
Msimamizi wa nyumba hiyo Bi. Elizabeth Andrea (mtoto wa mwenye nyumba) akizungumza kwa niaba ya baba yake mzazi amesema mpangaji huyo amekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoa lugha chafu mbele ya wapangaji wezake sambamba na kutolipa kodi kwa wakati akibainisha kuwa anadaiwa kodi ya miezi 8 hadi sasa.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Msalala road Bw. Sostenes Calist amekiri kupokea malalamiko hapo awali juu ya mpangaji huyo kuchelelewa kulipa kodi na kwamba alipewa andiko maalumu la kuhama katika nyumba hiyo.