Wezi waiba ng’ombe kisha kuchinja usiku mtaa wa Magogo A
15 January 2025, 10:25 am
Matukio ya wizi katika mtaa wa Magogo A kata ya Buhalahala manispaa ya Geita mkoani Geita yadaiwa kuwa mwiba kwa wakazi wa eneo hilo ambapo kwa sasa hofu imetanda.
Na: Paul William – Geita
Familia nne tofauti katika mtaa wa Magogo A kata ya Buhalala manispaa ya Geita zimejikuta katika wakati mgumu baada ya kuibiwa mifugo yao (ng’ombe) kwa nyakati tofauti tofauti majira ya usiku.
Wakizungumza na Storm FM baadhi ya wafugaji katika mtaa huo wamesema matukio hayo ya kuibiwa ng’ombe yametokea kwa kufuatana na yote yakifanyika katika mtaa mmoja.
Reiberatus Ngovongo ni mfugaji na hakimu mstaafu anayeishi katika mtaa huo ambaye ni miongoni mwa walioibiwa ng’ombe iliyokuwa na mimba ambayo ilichinjwa usiku wa kuamkia Januari 11, 2025 ndani ya shamba lake la mahindi na kisha nyama kuchukuliwa.
Akizungumzia suala hilo mke wa mzee Ngovongo anafafanua namna ambavyo walianza msako baada ya kubaini kuwa wameibiwa mfugo.
Familia nyingine zilizoibiwa ni ya Marekana na ya mwenyekiti mstaafu ambapo wakizungumza wake wa familia hizo wamebainisha namna walivyogundua taarifa ya kuibiwa.
Kufuatia changamoto hiyo, kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamekiri kuwa jambo hilo limeendelea kushamiri na kuomba uongozi kuona namna ya kuweza kudhibiti.
Balozi wa Magogo shina namba mbili Bw. Petro Gasiri amekiri kutokea kwa tukio hilo katika eneo lake huku mwenyekiti wa mtaa huo Juma Ramadhani akizungumza kwa njia ya simu amesema hawezi kueleza jambo hilo kwa simu na kutoa muda ambao watakuwepo ofisini kwake kwaajili ya kutolea ufafanuzi jambo hilo.