Kaka wa marehemu adaiwa kumfukuza mjane na watoto Geita
9 January 2025, 10:23 am
Miongoni mwa changamoto zinazoendelea kuwakabili wajane mkoani Geita ni pamoja na suala la mirathi ambapo wakati mwingine wamekuwa wadhurumiwa.
Na: Paul William – Geita
Mjane wa aliyekuwa diwani wa kata ya Nyankumbu marehemu Michael Kapaya mkazi wa mtaa wa Shilabela Manispaa ya Geita mkoani Geita amelazimika kuomba msaada katika ofisi ya mtaa huo kwa kile kinachodaiwa kufanyiwa fujo na shemeji yake (kaka wa marehemu) aitwaye Andrea Kapaya akimshinikiza kutoka katika nyumba anayoishi mjane huyo pamoja na watoto wake.
Mama huyo amewasilisha malalamiko yake Januari 08, 2025 katika ofisi ya mtaa ambapo imeelezwa kuwa kaka huyo wa marehemu alizuia wapangaji katika nyumba hiyo kulipa kodi kwa mjane huyo aitwae Monika John na badala yake kodi apewe yeye na baadaye aliweka bango katika nyumba hiyo linalosema nyumba inauzwa (pichani) pasipo kumhusisha mjane huyo.
Baadhi ya wapangaji katika nyumba hiyo wameeleza kushangazwa na kitendo cha kaka wa marehemu kumfanyia fujo shemeji yake ambaye ndiye msimamizi halali wa nyumba hiyo na kuongeza kuwa inabidi wakae kuzungumza ili wamalize tofauti zao.
Mtoto wa marehemu ameiomba serikali iingilie kati suala hilo kwani wakitolewa katika nyumba hiyo hawana sehemu nyingine ya kwenda kuishi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Shilabela Fredrick Zingula Masalu amekiri kupokea malalamiko hayo na kueleza kuwa alimuandikia barua kwaajili ya kwenda kwa mkuu wa wilaya kwaajili ya utatuzi zaidi.