KKKT kuanzisha makanisa maeneo ya visiwani
30 December 2024, 4:03 pm
Licha ya maeneo ya visiwani kuwa na idadi kubwa ya watu kutokana na shughuli za uzalishaji mali kama uvuvi bado maeneo hayo yanakumbana na changamoto ya ukosefu wa nyumba za ibada.
Na: Edga Rwenduru- Geita
Kufuatia changamoto hiyo, kanisa la Kiinjili la kirutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya mashariki ya ziwa viktoria imeanzisha utaratibu wa kuanzisha makanisa katika maeneo ya visiwani ili kuwapa nafasi watu wanaofanya shughuli katika maeneo hayo kuweza kuabudu.
Askofu msaidizi wa Dayosisi hiyo Stephano Ling’wa akiwa katika kongamano la vijana wa kanisa hilo mkoani Geita Disemba 29, 2024 amesema kanisa hilo limelenga kuvifikia visiwa vyote vilivyopo katika ziwa viktoria ndani ya miaka mitatu ijayo huku vijana wakipewa nafasi kubwa ya kufanya kazi hiyo.
Mchungaji Emmanuel Sita ambaye ni mratibu wa vijana KKKT Dayosisi ya mashariki ya ziwa viktoria na mchungaji Frank Mekson mratibu wa vijana KKKT Taifa wamesema wapo tayari kuwahamasisha vijana kuwa kipaumbele katika kazi hii ya kuanzisha makanisa maeneo yayanayohitaji huduma ya neno la Mungu.
Mchungaji kutoka usharika wa sayuni Mwatulole Elias Mganya ambaye pia ni mchungaji mlezi wa vijana amesema kanisa hilo linawajengea msingi mzuri vijana wa kufanya kazi ya Mungu wakiwa bado na afya njema.