RTO Geita atoa rai kwa madereva kipindi cha sikukuu
20 December 2024, 4:12 pm
Watumiaji wa vyombo vya moto mkoani Geita wameaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ili kupunguza ajali za barabarani.
Na: Kale Chongela – Geita
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Geita mrakibu wa Polisi (SP) Aloyce Jacob amesema jeshi hilo halitawafumbia macho baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wanaovunja sheria za usalama barabara.
Mrakibu Jacob ametoa kauli hiyo leo Disemba 20, 2024 akiwa katika kipindi cha Storm asubuhi cha Storm FM wakati wa mahojiano maalumu kuhusu kuimarisha usalama barabrani kuelekea katika sikukuu za mwisho wa mwaka huku akiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kutoendesha mwendo kasi sambamba na kuzidisha abiria.
Katika hatua nyingine amewaasa abiria kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi waonapo vitendo vya ukiukwaji wa usalama barabarani kwani itasaidia kupunguza wimbi la ajali.
Afande Jacob amesema katika kuonesha jeshi hilo liko kazini kwa mwaka 2024 wamefungia leseni 26 za madereva kwa kukiuka sheria za usalama barabarani n akuwaonya wengine wanaondelea kukiuka sheria hizo.