Wasafirishaji abiria kwa boti wasisitizwa kuzingatia sheria
28 November 2024, 3:10 pm
Baadhi ya maeneo mkoani Geita yamekuwa na shughuli mbalimbali za majini ikiwemo uvuvi pamoja na kusafirisha abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wamiliki wa boti za abiria zinazofanya safari kutoka kata ya Nkome mkoani Geita kuelekea katika visiwa mbalimbali vilivyopo katika ziwa viktoria wametakiwa kuacha tabia ya kuzidisha idadi ya abiria na mizigo kwani ni hatari kwa maisha ya abiria.
Maagizo hayo yametolewa na Godfrey Chegele ambaye ni afisa mfawidhi wa shirika la uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) mkoa wa Geita alipotembelea katika mwalo boti za abiria Nkome ambapo amesema kipindi hiki cha mwisho wa mwaka baadhi ya boti zinakiuka utaratibu wa usafari wa majini kwa kuzidisha abiria na mizigo kwa kiwango kisichotakiwa.
Aidha Chegele amewahimiza abiria wanaotumia vyombo vya majini kuzingatia suala la usalama kwa kuhakikisha kila mmoja anavaa maboya kabla ya kuanza safari.
Aidha kwa upande wao wavuvi wa mwalo wa Makatani wamesema wamejiwekea utaratibu wa kuwadhibiti baadhi ya wavuvi wanaoingia ziwani wakiwa wamelewa.