Storm FM

Rufaa 56 kati 57 za CHADEMA zakubaliwa Geita

19 November 2024, 12:01 pm

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Geita mjini akizungumzia rufaa zilizowasilishwa kwenye ofisi yake. Picha na Edga Rwenduru

Baada ya mchakato wa kuwasilisha rufaa kupinga kuenguliwa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa hatimae mbivu na mbichi zimejulikna

Na Edga Rwenduru:

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Geita mjini Yefred Myenzi amesema walipokea jumla ya rufaa 57 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na kati ya hizo rufaa 56 zimekubaliwa na moja imekataliwa.

Myenzi ambaye pia ni mkurugenzi wa halmshauri ya mji wa Geita amesema hayo akiongea na Redio Kwizera ofisi kwake juu ya mchakato uliofikiwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakayofanyika Novemba 27, 2024

Aidha kwa vyama vingine walipokea rufaa moja kutoka chama cha ACT wazalendo na rufaa moja kutoka chama cha wananchi CUF na zote zimekubaliwa.

Hata hivyo Myenzi amewataka wananchi kuacha imani potofu kuwa hawawezi kuchagua watu ambao baadaye hawatatangazwa huku akisisitiza kuwa, kura za wananchi ndio huamua matokeo.

Ikumbukwe kuwa, kampeni zitaanza Novemba 20 hadi Novemba 26 ambapo uchaguzi utafanyika Novemba 27.