GGML yakabidhi pikipiki 50 kwa Jeshi la polisi Geita
22 October 2024, 5:38 pm
GGML imeendelea kushirikiana na serikali katika kufadhili shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani Geita ikiwa ni ajenda yao ya kunufaisha Jamii inayozunguka mgodi huo.
Na: Ester Mabula – Geita
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imekabidhi pikipiki 50 kwa Jeshi la polisi mkoa wa Geita zenye thamani ya shilingi milioni 175 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuimarisha usalama na ulinzi wa mkoa.
Hafla ya makabidhiano imefanyika katika ukumbi wa bwalo la polisi uliopo halmashauri ya mji wa Geita ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, viongozi wa mkoa, viongozi wa GGML pamoja na watendaji wa Jeshi la polisi.
Mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni ameupongeza mgodi wa GGML kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu akieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji kazi kwa Jeshi la polisi.
Makamu wa Rais mwandamizi wa Anglo Gold Ashanti Afrika Terry Strong amesema GGML inaendelea kutambua kazi kubwa inayofanywa na polisi na hivyo wataendeleza ushirikiano ili kurahisisha utendaji kazi huku Afisa mwandamizi wa mahusiano Gilbert Moria akieleza kuwa GGML itaendelea kunufaisha Jamii inayozunguka mgodi huo.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela ameipongeza GGML kwa kuendelea kutoa ufadhili katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kuahidi kuendeleza kudumisha ushirikiano kwa maendeleo ya mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla.
Baadhi ya askari polisi wamesema pikipiki hizo zitawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku sambamba na kudumisha usalama wa raia.
GGML imeendelea kudumisha ushirikiano na serikali ambapo kupitia miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa Jamii (CSR) imekuwa ikitenga shilingi Bilioni 1.9 kila mwaka kwaajili ya utekelezaji wa miradi.