Ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Buhalahala waanza
28 September 2024, 9:46 am
Wana-CCM kata ya Buhalahala wameanza mchakato wa ujenzi wa ofisi ya chama hicho katika kata hiyo ili kuondoa changamoto ya muda mrefu ya kukosa ofisi.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wanachama wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Buhalahala iliyopo wilayani Geita wameshiriki kwa pamoja katika uchimbaji wa msingi kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho inayojengwa katika mtaa wa mwatulole.
Wakizungumza na Storm Fm wanachama hao wamesema endapo ujenzi wa ofisi hiyo utakamilika utaenda kutatua changamoto ya wanachama kupata huduma kwa urahisi kwani hata mikutano ya chama ilikuwa wanalazimika kuifanyia chini ya miti.
Mwenyekiti wa Chama hicho kata ya Buhalahala Mwisa Elias Kabese pamoja na John Mwanda ambaye ni mtaalamu anayesimamia ujenzi wa ofisi hiyo wamesema ujenzi wa ofisi utagharimu zaidi ya milioni 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
Naye Mwenezi wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Geita Gabriel Nyansilu ambaye alikuwa mgeni rasimi katika uzinduzi wa ujenzi huo pamoja na Manjale Magambo mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Geita wamewataka wananchama wa chama hicho kata ya Buhalahala kuzidisha ushirikiano.