Storm FM

Theresia (18) aliyeuawa kwa risasi azikwa Kashelo

13 September 2024, 8:11 pm

Wakazi wa Kata ya Lulembela wakiwa katika mazishi ya Theresia John aliyeuawa kwa risasi. Picha na Mrisho Sadick

Hatimae mwili wa Theresia John aliyeuawa katika vurugu za wananchi na jeshi la polisi Kata ya Lulembela wilayani Mbogwe Mkoani Geita umezikwa.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amewaonya wakazi wa Kata ya Lulembela wilayani Mbogwe kuacha tabia ya Kujichukulia Sheria mkononi kwani vitendo hivyo vimekuwa vikichangia mauaji kwa watu wasiyo husika.

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya msichana Teresia John (18), Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Lulembela aliyeuwawa Kwa kupigwa risasi katika vurugu za Wananchi zaidi ya 800 kuvamia Kituo hicho Cha Polisi Lulembela kwa nia ya kuwachukua kwa nguvu watuhumiwa wa wizi wa watoto.

Maziko hayo yamefanyika katika kitongoji cha Kashelo kata ya Lulembela huku mkuu wa wilaya ya Mbogwe Sikina Mohamed ameishukuru familia iliyokumbwa na mkasa huo kwa kuipatia serikali ushirikiano huku akiwataka wananchi kuendelea kuishi kwa kufuata sheria za nchi ili kuepuka kuwa sababu ya matatizo kwa watu wengine.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mkuu wa wilaya Mbogwe
Mkuu wa mkoa wa Geita akizungumza na waombolezaji msibani Lulembela. Picha na Mrisho Sadick

Diwani wa Kata ya Lulembela Deus Lyankando amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Geita kurejesha huduma za kipolisi kwakuwa tangu uvamizi huo ufanyike hakuna huduma hizo huku mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbogwe akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwakamata wote waliohusika katika vurugu hizo.

Sauti ya diwani na mwenyekiti wa CCM Mbogwe

Hata hivyo kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la polisi nchini imesema ilibainika Watu waliokuwa wamebeba Watoto hao ni Emanuel John (33) Mkazi wa Kigamboni Lulembela ambaye alikuwa amembeba Mtoto wake aitwaye Ikram Emanuel na wa pili anaitwa Ng’amba Leonard (24) ambaye alikuwa amembeba Mtoto aitwaye John Emanuel, Mama wa Watoto hao aitwaye Rachel Masunga Luhende (22) Mkazi wa Kigamboni Lulembela amethibitisha kuwa Watoto hao ni wa kwake.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa msibani katika kitongoji cha Kashelo. Picha na Mrisho Sadick

Katika tukio hilo lililotokea Septemba 11,2024  kijana mwingine mwenye umri wa miaka 20 aliuawa , Mwaka 2022 wakazi wa Kata hiyo waliwashambulia nakuwaua askari wawili wa Uhamiaji huku serikali ikionya tabia hizo.