mama
Storm FM

Risasi ya polisi yadaiwa kusababisha kifo Lulembela

12 September 2024, 7:20 pm

Pichani ni Mama mzazi wa Teresa John binti aliyeuawa katika vurugu za polisi na wananchi. Picha na Evance Mlyakado.

Vurugu za wananchi na polisi katika kituo cha Polisi Lulembela wilayani Mbogwe zasababisha vifo vya watu wawili.

Na Evance Mlyakado:

Watu wawili wamefariki dunia katika kata ya Lulembela wilayani Mbogwe Mkoani Geita baada ya vurugu zilizoibuka na kupelekea watu zaidi ya 800 kuvamia kituo cha Polisi wakiwatuhuhumu watu wawili kuwa ni wezi wa watoto kwakuwa walionekana wamebeba watoto wawili.

Waliofariki dunia katika vurugu hizo ni mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 20 na wa pili ni Msichana aitwaye Teresia John mwenye umri wa miaka 18, Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lulembela.

Ndugu wa familia ya akiwemo mama mzazi wa mtoto huyo amesema mtoto wake alifikwa na umauti huo akiwa ndani ya chumba chake baada ya risasi kupenya dirishani nakumpiga..

Sauti ya mama mzazi wa mtoto pamoja na ndugu wa familia.

Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lulembela Maisha william Maginya amesema tukio hilo la kusikitisha ni la kwanza kutokea kijijini humo huku akitoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwakuwa ni hatari kwa maisha ya watu wengine.

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji
Serikali ya wilaya hiyo imeahidi kugharamia mazishi ya watu hao waliofariki katika vurugu hizo huku Jeshi la polisi limesema bado linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Gari lililochomwa moto na wananchi wenye hasira kali katika vurugu hizo. Picha na Evance Mlyakado

Taarifa iliyotolewa September 11,2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema “Chanzo cha tukio hilo ni baada ya Watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba Watoto wawili na Wananchi waliokuwa katika mnada wa Lulembela kuwahisi kuwa ni Wezi wa Watoto na kuanza kuwashambuilia, akatokea Mtendaji wa Kata akawabeba kwenye pikipiki na kuwakimbiza Kituo cha Polisi Lulembela”

“Wananchi wanaokadiriwa kufikia 800 walifika kituoni hicho na kuwataka Askari wawakabidhi Watuhumiwa ili wawaue”
“Wananchi hao walianza kushambulia Kituo cha Polisi kwa mawe wakilazimisha kuwachukua Watu hao kwa nguvu ili wawaue, mbali na kushambulia kituo hicho kwa mawe na kutaka kuingia kwa nguvu ndani ya kituo hicho, Wananchi hao walichoma moto gari moja lilioegeshwa nje ya kituo hicho.

Muonekano wa kituo cha polisi Lulembela kilichoshambuliwa na wananchi. Picha na Evance Mlyakado.

Ilibainika Watu waliokuwa wamebeba Watoto hao ni Emanuel John (33) Mkazi wa Kigamboni Lulembela ambaye alikuwa amembeba Mtoto wake aitwaye Ikram Emanuel na wa pili anaitwa Ng’amba Leonard (24) ambaye alikuwa amembeba Mtoto aitwaye John Emanuel, Mama wa Watoto hao aitwaye Rachel Masunga Luhende (22) Mkazi wa Kigamboni Lulembela amethibitisha kuwa Watoto hao ni wa kwake.