Mkandarasi atelekeza mradi wa maji Katoro
6 September 2024, 7:32 am
Serikali kupitia wakala wa usambazaji maji vijijini (RUWASA) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kuondoa changamoto kwa wananchi katika wilaya ya Geita.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba amefanya ziara ya kukagua miradi mitatu ya maji katika kata za Nyarugusu na Katoro yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.
Akikagua miradi hiyo DC Komba amebaini changamoto ya mkandarasi Jefa Investment anayetekeleza ujenzi wa tenki la maji katika mradi wa maji uliopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro kudaiwa kuutelekeza mradi huo hali iliyopelekea mradi kushindwa kukamilika kwa wakati.
Diwani wa kata ya Katoro Benedict Sweya ameeleza juu ya chanagmoto hiyo kuwa mkandarasi haonekani na pia kupitia mawasiliano yake amekuwa hapatikani.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama na ujenzi wa mradi huo ulitarajiwa kuwaondolea changamoto hiyo.