Geita yaanza zoezi la uandikishaji wapiga kura
6 August 2024, 11:58 am
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, mkoa wa Geita umeanza zoezi la uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura.
Na: Kale Chongela – Geita
Zoezi la uandikishaji na uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura limeanza Agosti 05, 2024 katika mkoa wa Geita, huku mwitio wa wananchi ukiwa hauridhishi kwa baadhi ya maeneo.
Afisa mtendaji wa mtaa wa Moringe kata ya Buhalahala katika halmashauri ya mji wa Geita akiwa katika shule ya sekondari Kalangalala ambapo pia kuna kituo cha uandikishaji na uboreshaji wa taarifa, amewasihi wananchi kujitokeza ili waweze kujiandikisha sambamba na kuboresha taarifa zao.
Katibu mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Bw. Ado Shaibu Ado akiwa mkoani Geita amesema ili mwananchi aweze kushiriki kwenye uchaguzi wa kiongozi amtakaye ni lazima aweze kujiandikisha sambamba na kuboresha taarifa zake.
Baadhi ya wananchi waliofika kwaajili ya zoezi hilo wamewahimiza wananchi wengine kujitokeza ili kuweza kuboresha taarifa zao.
Vituo vya kuandikisha wapiga kura katika mkoa wa Geita ni 1637 huku idadi ya wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa kwa mkoa wa Geita ni 299,672.
Zoezi la kuandikishwa litadumu kwa muda wa siku 7 ambapo limeanza Agosti 05, 2024 na linatarajia kukamilika Agost 11 mwaka huu.