GGML yawapiga msasa madereva wa serikali Geita
1 August 2024, 3:08 am
Kampuni ya GGML imeendelea kuiishi dhana ya kuwa usalama ni tunu namba moja inayoendesha shughuli zote za ndani na nje ya mgodi na hivyo kusaidia jamii kuwa na tabia chanya za kuzingatia usalama.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Geita Gold Mining limited (GGML) kwa kushirikiana na ofisi ya katibu tawala mkoa wa Geita imeendesha warsha ya mafunzo ya siku nne kuhusu usalama barabarani kwa madereva wa serikali zaidi ya 40 katika halmashauri ya mji wa Geita na halmashauri ya wilaya ya Geita kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika katika ukumbi wa EPZA eneo la uwekezaji Bombambili mjini Geita, msimamizi wa ushirikishaji wa wadau Elibariki Jambau amesema kuwa mafunzo hayo ni kutokana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria za barabarani kwa baadhi ya madereva unaopelekea ajali za barabarani.
Meneja wa idara ya ulinzi ndani ya GGML Sylvester Rugaba aliyemwakilisha meneja wa mgodi wa GGML, amesema GGML kupitia tunu ya usalama katika maeneo ya kazi imeamua kuendesha warsha hiyo ili kukabiliana na vitendo vya mwendokasi katika aeneo yote ya barabara.
Mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Geita Aloyce Jacob amewaonya madereva wa serikali kuachana na tabia ya kutozingatia sheria na alama za usalama barabarani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa madereva wa serikali Steven Kachungwa na baadhi ya madereva waliohudhuria warsha hiyo wameeleza umuhimu wa mafunzo hayo na changamoto wanazozipitia katika kazi zao.
Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Geita Dkt. Elphace Msenya aliyemwakilisha katibu tawala wa mkoa wa Geita Mohamed Gombati kama mgeni rasmi amewataka madereva kuunda umoja wao utakaowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.