Uchomaji taka kiholela wawaibua wakazi wa Mbugani na Msalala road
23 July 2024, 2:53 pm
Suala la uchafuzi wa mazingira limeendelea kupigwa vita ili kuhakikisha kuwa Jamii inakuwa salama na kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.
Na: Amon Bebe – Geita
Baadhi ya wananchi wa mitaa ya Mbugani na Msalala road halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita wamewalalamikia watu ambao wamekuwa na tabia ya kukusanya taka na kuzichoma moto badala ya kuzipeleka kwenye madampo ambayo yamewekwa na halmashauri kwaajili ya taka hizo.
Wakizungumza na Storm Fm kwa nyakati tofauti Julai 22, 2024 wananchi hao wamesema uchomaji wa taka hizo unasababisha moshi na harufu mbaya kwenye maeneo yao ya makazi pamoja na Biashara zao.
Kwa upande wa baadhi ya wananchi wametetea kitendo hicho wakidai kuna wakati madampo yanakuwa yemejaa na magari ya taka ya halmashauri na kwamba hayapiti kwa wakati kuchukua taka.
Mwenyekiti wa mtaa wa Msalala road Sostenes Kalist amesema wananchi wana elimu ya usafi wa mazingira na wanaelewa kuwa kuchoma taka ni kinyume na utaratibu na kuwaasa waendelee kufuata utaratibu vinginevyo watachukuliwa sheria kwa wale watakao kaidi.
Akizungumza kwa njia ya simu na Storm FM, afisa mazingira kutoka halmashauri ya mji wa Geita Edward Chacha Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananci juu ya uhifadhi wa taka.