Wakazi wa Narusunguti walia na ukosefu wa maji safi na salama
10 July 2024, 9:49 am
Licha ya mikakati ya serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kila kijiji, bado hali tete kwa wakazi wa kijiji cha Narusunguti wilayani Bukombe mkoani Geita wakiwa na changamoto hiyo tangu mwaka 2002.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Wananchi wa kijiji cha Narusunguti kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama hali inayowalazimu kufuata huduma hiyo wilaya jirani ya Chato.
Wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 09, 2024 wa kusomewa mapato na matumizi ya kijiji wameeleza namna wanavyopitia changamoto ya kupata huduma hiyo.
Diwani wa kata ya Busonzo kilipo kijiji hicho Safari Nicklas Mayala amethibitisha kuanzishwa kwa utafiti na uchimbaji wa visima vya kina kirefu vya maji vitakavyosaidia upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapo.
Awali, akisoma taarifa ya mapato na matumizi afisa mtendaji wa kijiji hicho Herman Martine Misinzo alibainisha hatua zilizoanzishwa na wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) katika kuhakikisha kuwa wananchi hao wanaondokana na changamoto hiyo huku mwenyekiti wa kijiji hicho akiwaasa wananchi kuendelea kuvumilia wakati serikali ikitatua kero hiyo.