Watu wanne wakamatwa na mali za wizi Geita
25 June 2024, 1:12 pm
Licha ya jitihada za Jeshi la polisi mkoani Geita kuendelea kuimarisha ulinzi, bado vitendo vya wizi na uporaji vinaendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo mkoani Geita.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Watu wanne akiwemo Ezekieli Misalaba maarufu kama ‘Mr. Masamaki” mkazi wa Nyankumbu wanashikiliwa na Jeshi a polisi mkoani Geita kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi katika mitaa mbalimbali mjini Geita.
Watuhumiwa hao wakiwa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita wametiwa nguvuni na jeshi la polisi katika operesheni iliyofanyika Juni 22, 2024 ambapo katika operesheni hiyo zaidi ya baiskeli 30, magodoro, redio na vitu vingine mbalimbali vimekamatwa.
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Geita, Kamishina msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi (SACP) Safia Jongo amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kubainisha hatua sitahiki zilizochukuliwa na jeshi hilo.
Awali katika mtaa wa Mwabasabi ambapo vitu vingi viliweza kukamatwa kwenye nyumba ya mmoja kati ya watuhumiwa hao wanne, wananchi na majirani wameonesha kushangazwa na tukio hilo kwani hawakutarajia kama jirani yao angekuwa akijihusisha na vitendo vya wizi.