Biteko atembelea banda la GGML maonesho ya OSHA
29 April 2024, 3:18 pm
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri mkuu na waziri wa nishati Dkt. Dotto Biteko ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kufanikiwa kudhibiti matukio ya vifo na majeruhi katika shughuli za uchimbaji mgodini na kuwasisitiza waajiri wengine kuhakikisha wakati wote wanalinda usalama wa waajiriwa wao.
Biteko ametoa kauli hiyo jana April 28, 2024 baada ya kutembelea banda la GGML katika maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yanayoendelea kwenye viwanja vya General tyre jijini Arusha.
Biteko ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo, ameeleza kufurahishwa na elimu ya afya na usalama mahali pa kazi inayotolewa na washiriki wa maonesho hayo.
“Niwapongeze wale mliofanya maonesho hapa, mmetoa elimu kubwa kwangu na kwale ambao tumepita lakini tumejifunza bado zipo kazi za kufanya,” – Biteko
Amesisitiza kuwa waajiriwa wanatakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi kwani kifo cha mtu mmoja kwa takwimu ni sawa na asilimia 100 kwa wategemezi wake ambao ni mke, watoto, ndugu na hata majirani.
Aidha ametoa wito kwa kila mtu kuthamini maisha yake na kwamba pindi anapokuja kazini arejee salama bila kuwa na madhara yoyote.
Awali akimkaribisha Dkt. Biteko katika banda la GGML, meneja usalama wa kampuni hiyo Isack Senya amesema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 hapajawahi kutokea tukio la vifo kwa mfanyakazi akiwa kazini.
Aidha, Senya pia alimueleza Dk. Biteko namna GGML inavyotumia mfumo wa rada kuangalia mienendo ya miamba au kuta katika maeneo ya uchimbaji.
Pia alimueleza kuwepo kwa chumba maalumu cha uokozi ambacho huwepo chini ya ardhi katika migodi ili kufanya uokozi pindi kunapotokea dharura yoyote.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA), Hadija Mwenda alisisitiza kuwa wataendelea kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.