Familia zaidi ya 20 zaathiriwa na mafuriko Geita
8 April 2024, 9:13 pm
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita na nchi nzima kwa ujumla, athari mbalimbali zimeendelea kujitokeza kwa wananchi ikiwemo kuharibika kwa miundombinu ya barabara na athari nyinginezo katika mazingira.
Na Evance Mlyakado – Geita
Mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumapili katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita, imeziacha familia zaidi ya 20 zilizopo mtaa wa Mbugani kata ya Kalangalala, halmashauri ya mji wa Geita katika hali ya sintofahamu kutokana na makazi yao kuvamiwa na maji.
Wakizungumza na Storm fm wananchi hao wamesema kuwa maji hayo yamezingira makazi yao baada ya mtaro unaopitisha maji kutoka katika daraja lililopo barabara kuu ya lami kupasuka na maji kusambaa katika makazi yao hali iliyosababisha wengi wao kushindwa kupika na kupata sehemu ya kujihifadhi.
Kwa upande wake meneja wa TARURA wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Subeya amesema kuwa shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa kandokando ya mtaro huo na wananchi wa maeneo hayo ndio zimesababisha mtaro huo kupasuka na maji yake kuvamia makazi hayo licha ya onyo na makatazo kadhaa kutolewa na serikali.