Sekta ya madini kutengeneza mabilionea wanawake nchini
2 October 2023, 10:44 am
Sekta ya Madini imeendelea kukua kila siku huku kundi la wanawake likionesha nia kubwa ya kuwekeza katika sekta hiyo huku serikali ikiahidi kuwapa kipaumbele.
Na Mrisho Sadick:
Chama cha wachimbaji wadogo wanawake nchini TAWOMA kimeanzisha Tuzo za Malkia wa Madini ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha juhudi za uwekezaji wa wanawake kwenye sekta ya madini huku chama hicho kikiwa kimetimiza miaka 25 tangu kianzishwe.
Akiwa katika hafla ya kitaifa ya kwanza ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Mkoani Geita nakuhudhuriwa na Waziri wa Madini, Mwenyekiti wa Chama hicho amesema wamedhamilia kuzalisha mabilionea wanawake wengi kupitia madini.
Mshindi wa Tuzo ya Malkia wa Madini 2023, Alice Kyanila amekiri tuzo hiyo ni kampeni sahihi kuwainua wanawake kuwa washindani kwenye sekta za madini na kuchangia mapato makubwa serikalini.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewahakikishia wachimbaji wanawake kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwawezesha kufanikisha uwekezaji wao kuanzia kwenye uchimbaji, uchenjuaji hadi sokoni huku Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amewataka kujipanga nakuweka mikakati ya kuanza uzalishaji mkubwa.