Geita Gold Queens yakwama, wadau waombwa msaada
24 August 2023, 8:30 pm
Ukata wa kifedha umekuwa changamoto kubwa kwa klabu mpya ya ligi kuu ya wanawake ya Geita Gold Queens ya hapa mkoani Geita, na kumuinua Mwenyekiti wa Chama cha Soka Geita kuwaomba wadau msaada.
Na Zubeda Handrish- Geita
Klabu ya wanawake ya hapa mkoani Geita iliyofanikiwa kupanda Ligi kuu kutokea Championship msimu ulioisha wa 2022/23 ya Geita Gold Qeens, hali imekuwa tofauti baada ya timu hiyo kushindwa kusajili hata mchezaji mmoja hadi sasa kwaajili ya msimu mpya.
Ikumbukwe Shirikisho la soka Tanzania TFF na Bodi ya Ligi Kuu TPLB siku chache zilizopita ilitoa orodha ya vilabu ambavyo havijasajili hata mchezaji mmoja hadi sasa huku Geita Gold Queens ikiwa miongoni mwao.
Mwenyekiti wa Chama cha soka mkoa wa Geita GEREFA, Salumu Kulunge ametolea ufafanuzi juu ya changamoto inayoikumba klabu hiyo ya soka ya wanawake ya mkoani hapa huku akiomba wadau kujitokeza kuisaidia.
Tukiwa tunajikumbusha katika shamra shamra za kuwapokea wana Geita Gold Queens baada ya kufanikiwa kupanda Ligi kuu, ambao huu msimu wa 23/24 ungekuwa msimu wao wa kwanza, alizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Zahara Michuzi kuhusiana na hatma ya klabu hiyo ya soka ya wanawake mkoani hapa.