Miili mitatu yatambuliwa wahanga wa ajali
13 July 2023, 9:16 pm
Majonzi yatawala wilayani Bukombe kufuatia ajali ya watu sita kufariki dunia, miili imeendelea kutambuliwa huku serikali ikitoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria.
Na Mrisho Sadick:
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Bukombe Mkoani Geita Dkt Timotheo Masota amesema kati ya miili sita ya marehemu waliyoipokea katika kituo cha afya cha uyovu kutokana na ajali ya Gari mitatu imetambuliwa na ndugu zao na imebaki mitatu.
Ajali hiyo imetokea Julai 13 , 2023 majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya gari dogo aina ya Toyota Haice lenye namba za usajili T 766 DQP kugongana uso kwa uso na Lori la mizigo katika kata ya Runzewe wilayani Bukombe Mkoani Geita.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishna msaidizi wa Polis ACP Safia Jongo akizungumza na Storm FM kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo nakwamba chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Haice kusinzia wakati akiwa mwendo kasi nakugongana na lori la mizigo.
Amesema miongo mwa watu waliofariki katika ajali hiyo ni Dereva wa Haice nakwamba majeruhi wawili wamefikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa uangalizi zaidi, huku akitoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani.