Watu wenye ulemavu waomba kipaumbele kwenye uchaguzi
23 November 2024, 10:59 am
Watu wenye ulemavu, wanawake na vijana wametakiwa kuhamasika kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba.
Na: Ester Mabula – Geita
Sikiliza simulizi ya Bi. Zainabu John (39) mwanamke mwenye ulemavu ambaye anaeleza harakati na jitihada ambazo amekutana nazo katika michakato ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na maisha yake ya siasa kwa ujumla.
Ili kuchangia katika kushughulikia changamoto za ushiriki wa wanawake, vijana, na watu wenyeulemavu katika michakato ya siasa, Kituo cha Demokrasia (TCD) kinatekeleza mradi wa mwakammoja ambao unalenga kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana kushiriki kwa ufanisi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ripoti ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 inaonyesha kuwa kati ya wenyeviti wa vijiji 11,915 waliochaguliwa, wanawake walikuwa 246 tu (sawa na 2.1%), huku wanaume wakiwa 11,669 (sawa na 97.9%).
Vilevile, kati ya wenyeviti wa mitaa 4,171, wanaume walikuwa 3,643 (87.4%) huku wanawake wakiwa 528 tu (12.6%). Aidha, kati ya wenyeviti wa vitongoji 62,612, wanaume walikuwa 58,441 (93.3%) na wanawake walikuwa wachache sana, 4,171 (6.7%).