Jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Geita yasaidia ujenzi wa shule
12 June 2024, 10:17 am
Jumuiya ya wazazi ya CCM ya wilaya ya Geita imeendelea na ziara ya kutembelea katika kata mbalimbali za wilaya hiyo ili kuzungumza na wanachama wake katika kuainisha na kutatua changamoto mbalimbali.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Jumuiya ya wazazi wilaya ya Geita imetembelea katika kata ya Isulwabutundwe na kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Ibisabageni ambapo changamoto mbalimbali ziliibuliwa na wananchi wa kijiji hicho.
Miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa ni pamoja na ukosefu wa shule ya sekondari kijijini hapo hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata masomo katika shule jirani ya Lubanga
Kutokana na changamoto hiyo jumuiya ilianzisha changizo fupi kwa lengo la kupata vifaa kadhaa vya ujenzi ambapo mifuko ya saruji 300 ilipatikana na pesa Tsh. 55,000.
Mwenyekiti wa shule ya msingi Ibisabageni Steven Pande akabainisha changamoto wanayoipata wanafunzi kutokana na kusomea shule hizo jirani.
Viongozi wa jumuiya hiyo, mwenyekiti wa jumuiya Robert Nyamaigoro na katibu elimu, malezi na mazingira Paschal Mapung’o katika changizo hilo wakahidi kuchangia katika ujenzi huo kwa kujenga darasa moja na kulikamilisha huku wakitoa mifuko 150 ya saruji.