Shule yenye walimu wawili wa bailojia yaongoza kiwilaya Geita
18 September 2023, 10:31 pm
Shule ya sekondari Lutozo iliyopo katika Mamlaka ya mji mdogo Katoro, ina walimu wawili wa bailojia ambao hulazimika kufundisha wanafunzi 2,049 yenye jumla ya mikondo 26 kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne.
Na Said Sindo- Geita
Shule hiyo ya kata, iliyopo mamlaka ya mji mdogo wa Katoro, wilayani na mkoani Geita, imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa miaka mitano mfululizo na mwaka jana ilikuwa ya kwanza kiwilaya kwa kufanya vizuri katika daraja la kwanza, daraja la pili na daraja la tatu katika mtihani wa kidato cha pili na kidato cha nne.
Mtaaluma wa shule hiyo, Ladislaus Jumanne Mkama anasema kwa mwaka jana jumla ya watoto 256 wa kidato cha nne waliokuwa wmesajiliwa, wote walifaulu kwa wastani wa asilimia 57 kwa kuanzia daraja la kwanza, daraja lapili na daraja la tatu isipokuwa mmoja pekee aliyepata sifuri.
Pamoja na kwamba changamoto wanazokutana nazo walimu na wanafunzi zinafanana kwa kiasi kikubwa, wanafunzi wanakabiliwa na matatizo mengi zaidi, ambayo ikiwa yatatuliwa mapema, yatakuza ubora wa elimu katika shule hiyo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Revocatus Maraha, anasema amekuwa akipokea simu kutoka Dar es salaam, Mbeya, Arusha na maeneo mengine ya nchi, wazazi wakiulizia nafasi za kuhamia huku wengine wakiuliza kama shule hiyo ni ya bweni.
Baadhi ya wanafunzi wamesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri wanakabiliwa na changamoto ya umbali mrefu, kukosa miundombinu ya maji na ukosefu wa bweni kwa wasichana hali inayohatarisha usalama wao kutokana na uwepo wa vishawishi vingi.