Wahofia ndoa zao kuvunjika chanzo ukosefu wa maji Nyankumbu
23 October 2024, 2:14 am
Wakazi wa mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu, halmashauri ya mji wa Geita, wameeleza kukumbwa na ukosefu wa maji kwa muda wa zaidi ya wiki mbili sasa
Na: Amon Mwakalobo – Geita
Kufuatia changamoto ya ukosefu wa maji kwa wakazi wa mtaa wa Uwanja, kwa sasa inawalazimu wakazi hao kununua dumu moja la maji kwa bei ya shilingi 200 hadi 500, hali inayowabana kiuchumi na kusababisha usumbufu katika shughuli zao za kila siku.
Baadhi ya wanawake wamesema wanahofia ndoa zao kuvunjika kwa sababu ya changamoto hiyo wakisema inawalazimu kuamka Alfajiri kwenda kutafuta maji na kuacha waume zao wamelala na changamoto inakuja wanapochelewa kurudi waume zao wanahisi mambo mengine.
Kwa upande wa wanaume waishio mtaa huo wamekiri kuwa changamoto ya maji mtaani hapo inawapa wakati mgumu sana kiasi kwamba wakati mwingine wanashindwa hata kuoga na kupiga miswaki.
Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Geita (GEUWASA) Frank Changawa amesema anaangalia utaratibu wa kurekebisha ratiba ili wananchi hao wapate maji angalau mara tatu kwa wiki.