Dereva agonga taa ya barabarani na kutokomea kusikojulikana
16 October 2024, 9:58 am
Kufuatia maboresho ya miundombinu ya barabarani katika mji wa Geita, wananchi wameaswa kuwa makini wakati wa utumiaji wa miundombinu hiyo.
Na: Kale Chongela – Geita
Wakala wa barabara nchini TANROADS mkoa wa Geita umetoa angalizo kwa madereva wanaoharibu miuondombinu ya barabara ikiwemo taa na alama za usalama zilizopo barabara.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 15, 2024 na mkuu wa kitengo cha matengenezo kutoka TANROADS mkoa wa Geita mhandisi Fredrick Mande kufuatia tukio la dereva kugonga taa ya barabarani katika mtaa wa Mwatulole halmashauri ya mji wa Geita lililotokea Oktoba 12, 2024.
Mhandisi Mwande amesema baada ya tukio hilo dereva wa gari aliitelekeza gari na kukimbia ambapo ameitaja gari hiyo kuwa ni aina ya Scania lenye usajili namba T 825 DQF.
Kwa upande wa watumiaji wa barabara wamesema kuwa kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja katika kulinda miundombinu ya barabara ili kuondoa changamoto ikiwemo ajali nyakati za usiku.