Hospitali ya rufaa ya kanda Chato yarahisisha huduma kupitia maonesho ya 6 Geita
25 September 2023, 8:42 am
Ukaribu wa huduma ya afya kwa wananchi unarahisisha mwamko wa wananchi katika kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu kwa wakati, hilo limesababisha Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kushiriki maonesho ya 6 ya kimataifa ya teknolojia ya madini.
Na Zubeda Handrish- Geita
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato imeendelea kuwa hitimisho la matibabu kwa wananchi wa Geita na mikoa mingine kwa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa, huku ikizidi kuwasogezea huduma karibu kupitia maonesho ya 6 ya kimataifa ya teknolojia ya madini.
Dkt. Liberias Libent kutoka Hospitali ya ya Rufaa ya Kanda Chato kutoka kitengo cha moyo amesema moja ya lengo ni kutoa huduma bure pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaofika katika maonesho hayo.
Baadhi ya huduma zinazotolewa katika banda la Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ni pamoja na kupima sukari na presha, kupima uwiano wa uzito na urefu, kupima viashiria vya magonjwa ya moyo na figo na kupima moyo, sambamba na kuelimisha wachimbaji wa madini kulinda afya.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamefika kwenye banda la Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato akiwemo Tumpe Jonas mkazi wa Geita na Stephano Peter kutoka Tabora wameelezea walivyofurahishwa na huduma zinazotolewa katika banda hilo.
Kupitia maonesho ya 6 ya Kimataifa ya teknolojia ya madini mwaka 2023 yenye kauli mbiu inayosema “Matumizi ya Teknolojia Sahihi Katika Kuinua Wachimbaji Wadogo kiuchumi na kuhifadhi mazingira, hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato imewasogezea karibu wananchi wa mkoa huu wa Geita na mikoa mingine huduma za uchunguzi na ushauri wa lishe bora pamoja na utunzaji mazingira dhidi ya magonjwa tunayoweza kuyapata kupitia mazingira tunayoishi hasa magonjwa sugu.