Shirika la ICAP latoa pikipiki 50 idara ya afya Geita
16 January 2025, 2:27 pm
Katika kuendelea kurejesha kwa jamii, shirika la ICAP limefadhili jumla ya pikipiki 50 kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani Geita.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Shirika la ICAP linalotoa huduma ya matibabu na matunzo kwa waathirika wa Virusi Vya Ukimwi nchini limekabidhi pikipiki 50 kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambazo zitawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naibu mkurugenzi mkazi wa shirika la ICAP Dkt. John Kahemele akizungumza na waandishi wa habari Januaria 14, 2025 mara baada ya kukabidhi pikipiki hizo kwa mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amesema shirika hilo pia limetoa mashine aina ya themo calculators kwaajili ya matibabu ya awali saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine shigela amelishukuru shirika hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii huku akiwaahidi ushirikiano kutoka kwa serikali kwani mkoa wa Geita unaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa maendeleo yakiwemo mashiriki ya kiraia katika kusaidia jamii.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt. Omary Sukari ameahidi kuwa atahakikisha pikipiki hizo zinatumika kwa lengo lililokusudiwa na siyo vinginevyo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo amepongeza hatua iliyofanywa na shirika hilo na kusisitiza wadau mbalimbali kuendelea kusaidia.