Watoto bado wanakabiliwa na changamoto Geita
20 October 2024, 8:09 pm
Watoto hususani wa kike mkoani Geita bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika jamii ikiwemo kutoaminiwa,nakupewa nafasi ya kufanya maamuzi.
Na Mrisho Sadick:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali imedhamiria kuboresha na kulinda ustawi wa watoto wote Tanzania na kupunguza athari zitokanazo na ukatili ,umasikini, afya na vifo.
Hayo yamebainishwa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt Omary Sukari kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani mjini Geita yaliyoratibiwa na shirika la Plan International kwa kushirikiana na serikali ambapo amesema serikali inaendelea kutekeleza mpango harakishi wa miaka mitano wa kuwekeza kwa vijana katika nyanja zote huku akiitaka Jamii kuendelea kuwapa nafasi watoto ya kutoa mawazo yao nakufanya maamuzi.
Akiwa katika maadhimisho hayo msimamizi wa miradi ya Plan International kanda ya ziwa Rwambali Majani amesema licha ya tukio hilo wamekuwa na matukio na miradi mbalimbali yenye lengo la kumwezesha mtoto kike kutimiza ndoto zake nakwamba shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali kikamilifu.
Mkuu wa Dawati la jinsia Kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Grace Mwaijage anasema bado wanaendelea kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto vinavyochochewa na mila na desturi huku Meneja mradi wa KAGIS unaofadhiliwa na serikali ya watu wa Canada Eliued Mtalemwa akisema katika mapambano ya kumwezesha mtoto wa kike kufikia malengo yake wamefadhili ujenzi wa vyoo zaidi ya 20 mashuleni pamoja na kuanzisha maabara ya hedhi salama yenye kutoa elimu kwa mabinti namna walio katika umri balehe.
Baadhi ya watoto wa kike waliopata nafasi ya kushiriki katika maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa kike duniani wamesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika jamii ya kubadili mtazamo juu ya mtoto kike kuwa anaweza kufanya kila kitu kama mtoto wa kiume huku wakilipongeza shirika la Plan International kwa kazi kubwa ya kubadili fikra na mitazamo hiyo katika jamii.