Naibu waziri wa Habari atoa maagizo kwa wakandarasi nchini
10 January 2024, 6:57 pm
Serikali ya awamu ya sita imejidhatiti katika kuimarisha mawasiliano nchini kwa kuongeza kasi ya ujenzi wa minara na vituo vya kuongeza nguvu ya mawasiliano.
Na Mrisho Sadick – Chato
Naibu Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandis Kundo Methew amewaagiza wakandarasi wote nchini wanaotekeleza ujenzi wa minara ya mawasilino 758 na vituo vya kuongeza nguvu ya mawasiliano kuhakikisha kufikia mwanzoni mwa mwaka 2025 kila mkandarasi awe amekabidhi mradi.
Mhandis Kundo ametoa maagizo hayo baada ya kukagua kituo cha kuongeza nguvu ya mawasiliano wilayani chato Mkoani Geita kinachojengwa kwa thamani ya bilioni 1.8 huku akisema serikali imejipambanua kuhakikisha inaboresha mkongo wa taifa kwa kutoa magari 45 yenye thamani ya bilioni 7.28 kwa ajili ya kuimarisha mkongo huo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Deusdedith Katwale amepongeza hatua hiyo huku akiiomba wizara hiyo kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano kwenye hifadhi za taifa zilizopo katika eneo hilo za Rubondo na Burigi Chato.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa TTCL Mkoa wa Kagera ambao unahudumia wilaya ya Chato Theopister Mark amesema mradi huo unalengo la kupanua huduma nakuongeza kasi ya mawasiliano huku diwani wa Kata ya Chato ulipo mradi huo Mange Ludomya akiipongeza serikali kwa hatua hiyo.