Serikali ya wilaya Geita yaagizwa kuongeza kasi usambazaji wa mbolea
17 October 2023, 10:25 am
Serikali imetakiwa kuharakisha mchakato wa usambazaji wa Mbole kwa wakulima kwakuwa wakulima wengi hususani katika wilaya ya Geita hawajafikiwa na mbolea hizo.
Na Mrisho Sadick
Chama Cha Mpinduzi CCM wilaya ya Geita kimeiagiza serikali ya wilaya ya Geita kusambaza kwa kasi pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kuwa idadi kubwa ya wakulima katika wilaya hiyo wanadai kutofikiwa na mbolea ilhali msimu wa kilimo umeshaanza.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka huu kufuatia baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya kata kudai kulalamikiwa na wakulima kutofikiwa na mbolea katika maeneo yao.
Awali kabla ya agizo hilo baadhi ya wajumbe walihoji kuhusu kasi ndogo ya usambazi wa mbolea huku Diwani wa Kata ya Bukoli Faraji Seif akiipongeza serikali kwa kufikisha kwa wakati pembejeo za kilimo katika Kata hiyo nakuwaomba wakulima kutumia fursa hiyo kulima kilimo chenye tija.
Afisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Malick Lugemalila amesema mpaka sasa wameshasambaza mbolea tani 48 nakwamba kufikia mwishoni mwa mwezi novemba mwaka huu watakuwa wamefikisha mbolea kwa wakulima wote wa halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe ameahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizoibuliwa katika kikao hicho huku mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholus Kasendamila akiwaonya baadhi ya wanachama wa chama hicho walioanza vurugu za kutafuta nafasi za Udiwani na Ubunge kabla ya mchakato halali kuanza.