Wafanyabiashara CCM Katoro waomba punguzo la kodi/ushuru
11 January 2025, 2:41 pm
Mwekezaji wa soko la CCM Katoro katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro alalamikiwa na wafanyabiashara katika soko hilo wakimtuhumu kutumia mabavu katika ukusanyaji wa kodi.
Na: Ester Mabula – Geita
Wafanyabiashara na machinga wanaofanya kazi katika soko la CCM Katoro katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani na mkoani Geita wamemlalamikia mwekezaji anayesimamia vizimba katika soko hilo kuwatishia kuwafukuza, kuwapandishia kodi ya vizimba sambamba na kutumia ubabe wakati wa ukusanyaji kodi.
Katika mkutano wa dharura ulioitishwa hivi karibuni na uongozi wa wafanyabiashara na machinga kata ya Katoro, wafanyabiashara hao wameeleza juu ya malalamiko hayo na kusisitiza kuwa hawamtaki mwekezaji huyo.
Akizungumzia suala hilo mwenyekiti wa wafanyabiashara eneo la CCM Katoro Misango Manyanda amemtaka mwekezaji huo kuzingatia sheria na si kutumia mabavu kwani tangu achukue tenda hiyo malalamiko yamekuwa mengi.
Diwani wa Kata ya Katoro Kigongo Swea amezungumzia sakata hilo na hapa anatoa ufafanuzi akiwasihi wafanyabiashara kuzingatia suala la mikataba yao katika eneo hilo.
Kwa upande wa Muwekezaji Rashid Sadick alipotafutwa kwa njia ya simu alieleza kuwa chama ndiyo chenye wajibu wa kuzungumzia suala hilo na si yeye.
Katika hatua ya kutafuta utatuzi juu ya mgogoro huo, Katibu wa CCM wilaya ya Geita Michael Msuya ameelekeza wafanyabiashara kufika katika ofisi yao kwaajili ya kutatua sambamba na kusikiliza pande zote mbili.