Storm FM

Mtoto (9) amwagiwa petroli na kuchomwa na mama yake kisa 800

3 December 2024, 2:58 pm

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo. Picha kutoka maktaba Storm FM

Mtoto wa kiume (9) mkazi wa kijiji cha Kasota kata ya Bugulula halmashauri ya wilaya ya Geita amejeruhiwa na mama yake mzazi baada ya kumwagiwa mafuta ya petroli kisha kumchoma moto kwa madai ya kuiba shilingi 800.

Na: Edga Rwenduru – Geita

Tukio hilo limetokea Disemba 2, 2024 katika kijiji cha Kasota, kata ya Bugulula ambapo mama wa mtoto huyo anadaiwa kumtuhumu mtoto wake kuiba fedha hiyo licha ya mtoto kukana kufanya kosa hilo na ndipo akaanza kumuadhibu kwa viboko kisha kumwagia mafuta na kumchoma moto hali iliyopelekea majeraha sehemu ya shingo, kifuani na mikononi.

Baada ya tukio hilo kutokea mtoto huyo alikimbizwa katika kituo cha afya Kasota na hali yake ilivyozidi kuwa mbaya alikimbizwa katika hospitali ya Nzera kwa matibabu zaidi, mama mdogo wa mtoto huyo Siwema Kulwa akiwa hospitalini hapo anazungumzia tukio hilo.

Sauti ya mama mdogo wa mtoto

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Nzera Shadrack Omega amesema baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitali alianza kupatiwa matibabu kwa uharaka zaidi na kwamba kwasasa anaendelea vizuri.

Sauti ya mganga mfawidhi

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo amethibisha kukamatwa kwa mama wa mtoto aliyetekeleza ukatili huo huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuadhibu watoto kupitiliza.

Sauti ya SACP Safia Jongo

Matukio haya yanaendelea kujitokeza licha ya Tanzania kuwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili na kwamba kwa takwimu zilizotolewa na Jeshi la polisi mkoa wa Geita katika uzinduzi wa maadhimisho hayo za kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu zinaonesha kupungua kwa matukio hayo kutoka 206 mwaka 2023 hadi 164 mwaka huu huku jamii ikitakiwa kuwa mstari wa mbele kukomesha vitendo hivyo.