Kero ya stendi Geita kujaa maji yatua baraza la madiwani
14 November 2024, 12:24 pm
Uduni wa miundombinu umetajwa kuwa changamoto ya kituo kikuu cha mabasi ya abiria mjini Geita kuzingirwa na maji kila msimu wa mvua huku mikakati ya kutatua changamo hiyo ikiwekwa.
Na Mrisho Sadick:
Siku chache baada ya mji wa Geita kukumbwa na mafuriko , baraza la madiwani wa halmashauri ya mji wa Geita limeiagiza halmashauri hiyo kutumia fedha za mapato ya ndani kufanya marekebisho makubwa kwenye Kituo kikuu Cha mabasi ya abiria ambacho huathirika kila msimu mvua kutokana na uduni wa miundombinu.
Katika kikao Cha Baraza la madiwani la Halmashauri ya mji wa Geita Cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu amewasilisha hoja ya dharura ya kuitaka Halmashauri hiyo kutenga fedha Kutoka mapato ya ndani kufanya marekebisho katika Kituo hicho licha ya uwepo wa mpango wa ujenzi wa kituo kipya kupitia mradi wa TACTIC.
Madiwani wa Kata ya Kalangalala Prudens Temba , Enock Mapande wa Kata ya Kanyara na Solome Ndekeja wa Kata ya Bulela wameunga mkono hoja hiyo kwa asilimia 100 huku wakisema watumiaji wa kituo hicho wanapata wakati mgumu nyakati zote iwe masiki au kiangazi huku wakiomba mchakato huo uwe wa haraka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Geita Yefred Myenzi ameipokea hoja hiyo kwa uzito wake huku Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Costantine Morandi akimtaka Mkurugenzi kuharakisha tathimini ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya Marekebisho hayo.