Huduma ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu yazinduliwa Chato
11 November 2024, 1:08 pm
Hospitali ya rufaa ya kanda Chato imeendelea kusogeza huduma za kibingwa ili kuwapunguzia mzigo wananchi wa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
Na Edga Rwenduru:
Kutokana na changamoto ya muda mrefu ya wananchi wa mkoani Geita na mikoa jirani kusafiri umbali mrefu kwenda Jijini Dar es salaam kufuata huduma ya matibabu ya mifupa,ubongo na Mishipa ya fahamu Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Chato kwa kushirikiana na hospitali ya MOI imezindua huduma hizo za kibingwa ili kutatua changamoto hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hizo za kibingwa uliofanyika katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Chato Dkt Oswald Lyapa mkurugenzi wa huduma za matibabu wa hospitali hiyo amesema uzinduzi wa huduma hizo umelenga kuwaondolea adha wananchi wa mkoa wa Geita ,Kagera na Kigoma ambao wilikuwa wanalazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma hizo hospitali ya Rufaa ya Bugando Jijini Mwanza.
Baadhi ya wananchi wamebainisha jinsi huduma hizo za kibingwa zitakavyo kwenda kuwasaidia kwani hapo awali walikuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo hali ambayo iliwafanya wengine kushindwa kutokana ugumu wa maisha nakusababisha kuwapoteza wapendwa wao.
Katibu tawala wa mkoa wa Geita Mohamed Gombati ambaye amezindua huduma hiyo ya matibabu ya kibingwa amewataka watumishi kutoa huduma kwa kuzingatia weledi wa kazi yao ili kuwasaidia wananchi wanaotoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupata huduma hapo.