Watishia kufunga barabara kutokana na mwendokasi wa bodaboda
9 October 2024, 9:48 am
Matukio ya ajali zinazosababishwa na mwendokasi wa baadhi ya madereva yawakera wananchi waishio maeneo ya Msufini mtaa wa Msalala road mjini Geita.
Na: Amon Mwakalobo – Geita
Baadhi ya wananchi wa maeneo ya Msufini Mtaa wa Msalala Road Halmashauri ya Mji wa Geita wametishia kufunga barabara inayounganisha mtaa huo na mtaa wa Nyankumbu kwa kuhofia kugongwa na kuumizwa na waendesha piki piki wanaondesha kwa mwendo kasi mtaani hapo bila kujali kuwa ni sehemu ya makazi ya watu.
Wananchi hao wamesema hayo leo Oktoba 09, 2024 wakizungumza na Storm FM kuwa baada ya kulimwa upya kwa barabara hiyo na kuwekwa molamu imepelekea waendesha pikipiki kukimbiza bila hata kufunga breki wanapoona wananchi na watoto wakivuka.
Mmoja wa wafanya biashara wa chakula (mama lishe) aliyejitambulisha kwa jina la mama Neema amesema mbali na mwendokasi wa waendesha pikipiki pia barabara hiyo ina vumbi sana kiasi kwamba tangia barabara hiyo ilimwe upya wamekuwa wakiugua mafua kila siku.
Baadhi ya waendesha pikipiki wanaoitumia barabara hiyo wamesema barabara hiyo sasa imekuwa mkeka na wanachojali ni kufika haraka huku wakieleza kuwa si wote wanaendesha kwa mwendo kasi.
Meneja TARURA wilaya ya Geita ambao ndio wasimamizi wa barabara za mita na vijiji Bi. Bahati Subeya amesema wataangalia utaratibu wa kuweka matuta katika maeneo ya makazi ya wananchi hao ili kuondoa adha wanayokumbana nayo.