Mapato ya madini ujenzi, Geita Mji yapaa
15 August 2024, 2:30 pm
Madini ujenzi ikiwemo mawe , kokoto , mchanga na moramu chanzo cha mapato kilichokuwa hakitazamwi sana katika halmashauri ya mji wa Geita.
Na Mrisho Sadick:
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita limempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kwa kuongeza kiwango cha makusanyo ya mapato kwenye madini ujenzi kwa kipindi cha mwezi julai.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Elias Ngole akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani Agosti 14,2024 amempongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kuongeza mapato kutoka katika chanzo cha madini ujenzi huku akimtaka kuendelea kupambana zaidi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Yefred Myenzi amesema kwa kipindi cha mwezi juni hadi julai wamekusanya zaidi ya milioni 20 kutoka milioni 2 iliyokuwa ikikusanywa hapo awali katika madini ujenzi huku siri ya mafanikio hayo ameeleza kuwa ni pamoja na kuongeza udhibiti.
Katika hatua nyingine Myenzi amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 halmashauri hiyo imepanga kukusanya zaidi ya bilioni 20 ikiwa ni sehemu ya bajeti ya halmashauri hiyo huku akiahidi kuendelea kubuni vyanzo vipya ili kuongeza mapato zaidi.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Costantine Morandi amesema licha ya halmashauri hiyo kupokea pesa zaidi ya bilioni 1 kutoka serikali kuu kwa ajili ya shughuli za maendeleo amemtaka mkurugenzi kuendelea kuongeza nguvu ya makusanyo ya mapato ya ndani nakukamilisha miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi.