Wachimbaji na wavuvi hawatumii vyoo kisa imani potofu
28 January 2024, 12:55 pm
Makundi ya wachimbaji na wavuvi yako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu kwasababu hawatumii vyoo kwenye maeneo yao.
Na Mrisho Shabani:
Wachimbaji wa madini ya dhahabu pamoja na wavuvi mkoani Geita wametajwa kuwa ni miongoni mwa makundi ambayo hayana utamaduni wa kutumia vyoo kutokana na imani potofu kuwa wakitumia vyoo uzalishaji wao unapungua.
Hayo yamebainishwa na Katibu tawala wa mkoa wa Geita Mohammed Gombati wakati wa ufunguzi wa kikao cha idara ya afya mkoani Geita kutathimini mafanikio na changamoto zinazoikumba idara hiyo huku akiagiza idara ya afya kuwekeza nguvu ya kutoa elimu kwa makundi hayo mawili.
Aidha kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dokta Omary Sukari ameagiza maeneo yote ya myalo pamoja na migodi lazima kuwepo na vyoo bora.
Uongozi wa Chama cha wachimbaji wadogo mkoani Geita GEREMA wameanza ziara ya kutembelea migodi ili kutoa elimu ya kuzingatia usafi maeneo ya migodini.