Naibu Waziri Kamani afunga maonesho ya Mufindi expo 2026
21 October 2026, 09:26

Na Fredrick Siwale
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amezitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa Wilaya ya Mufindi kwa kuandaa maonesho ya biashara na uwekezaji yanayolenga kukuza uchumi na kufungua fursa kwa wananchi.
Kamani ametoa wito huo wakati akifunga rasmi maonesho ya Mufindi Investment Forum and Expo 2026 yaliyofanyika wilayani Mufindi, mkoani Iringa, akimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Linda Salekwa, kwa ubunifu wa kuanzisha maonesho hayo.
Amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa kwa wananchi, ambapo zaidi ya watu 42,000 wamepata fursa ya kujifunza masuala ya uwekezaji, biashara, kilimo na uvuvi.
Aidha, Kamani amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa la kuwaunganisha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji, pamoja na kutoa elimu kuhusu fursa za kiuchumi na namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika shughuli zao za uzalishaji.
“Nikupongeze Mkuu wa Wilaya ya Mufindi kwa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa vitendo kupitia maonesho haya. Pia, nazielekeza wilaya nyingine kuiga mfano wa Mufindi,” amesema Kamani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, ameishukuru kamati ya maandalizi, kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wadhamini kwa mchango wao katika kufanikisha maonesho hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho hayo, Boniface Mliga, akisoma risala kwa mgeni rasmi, amesema jumla ya wananchi 42,300 wametembelea maonesho hayo na kupata elimu kuhusu sekta mbalimbali pamoja na kutambua fursa za kibiashara na uwekezaji.
Maonesho ya Mufindi Investment Forum and Expo 2026 yanatajwa kuwa jukwaa muhimu la kuchochea uwekezaji, kupanua fursa za biashara na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
