Nuru FM

Iringa: Twinsteps yaidhamini timu ya City Center

12 March 2024, 12:57 pm

Isaac Kikoti akiwa katika picha ya pamoja na kiongozi wa timu ya City Center Bw. Danny. Picha na Hafidh Ally.

Udhamini walioupata timu ya City Center utasaidia vijana wao kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Na Hafidh Ally

Kampuni ya Twinsteps inayojihusisha na kazi ya kuuza na kununua magari ndani na nje ya Tanzania imejitolea kuidhamini timu ya mpira wa miguu City Center ambayo ni timu ya vijana wanaotoka mitaani katika mazingira magumu na waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya na kuacha mkoani Iringa.

Msemaji wa kampuni ya Twisteps Isack Patrick Kikoti ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Iringa Mjini amesema kampuni hiyo ndio mdhamini rasmi wa timu ya City Center ambapo tayari wamewakabidhi vifaa vya michezo pamoja na mahitaji mengine muhimu.

Zaidi, Kikoti amesema timu hiyo ipo katika orodha ya timu zitakazoshiriki mashindano ya Simba Kihesa Super Cup mkoani Iringa, hivyo kampuni ya Twisted itatoa sapoti ya kutosha kuhakikisha maandalizi ya timu hiyo yanaenda vizuri ili waweze kufuzu katika michuano hiyo.

Sambamba na hilo, Kikoti amesema kupitia timu hiyo litafanyika Jukumu moja kubwa la kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya madawa ya Kulevya kwa vijana watakaojitokeza kwenye timu zitakazoshiriki mashindano hayo.

Kampuni ya Twisteps inajihusisha na kazi ya kuuza na kununua magari ndani na nje ya Tanzania ambapo hapa nchini Tanzania wananunua magari aina ya Land Cruiser wanazibadirisha ili ziwe na mwonekano mpya wa kupendeza kisha wanaziuza sehemu nyingine, lakini pia wanaagiza magari aina zote kutoka nchi za nje kuja Tanzania, makao makuu ya kampuni ya Twisted ipo Dar es salaam.