Nuru FM

Serikali yashauriwa kutoa fedha za kutosha kwa TARULA Mkoani Iringa

16 April 2021, 8:04 am

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Dkt. Ritta Kabati ameishauri serikali kuipatia fedha za kutosha wakala wa barabara Vijijini na Mijini TARULA ili ziweze kukarabati barabara za mkoa wa Iringa.

Mh. Kabati ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Hotuba ya waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuongeza kuwa TARULA ndio ambao wamekuwa wakisimamia barabara nyingi za vijijini hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele ili kuhakikisha barabara ambazo zimehabrika za mkoa wa iringa zinakarabatiwa.

Aidha amesema kuwa mpaka sasa kuna barabara za Wilaya ya Mufindi zimekuwa hazipitiki sambamba na wilaya ya kilolo ambazo zimekuwa ni kitovu cha uchumi wa mkoa wa Iringa.

Katika hatua nyingine Mh. Ritta kabati amebainisha kuwa ni vyema serikali ikawaajiri walimu ambao wamekuwa wakijitolea katika shule nyingi kwa kuwa wamekuwa chachu ya mafanikio ya mkoa wa iringa kukua kitaaluma.