Nuru FM

Polisi Iringa wafanya mdahalo wa ulinzi na usalama kwa wanahabari

24 November 2023, 3:11 pm

Wanahabari wakiwa na Polisi Mkoani Iringa kujadiliana kuhusu mahusiano katika kazi. Picha na Adelphina Kutika

Na Adelphina Kutika

Waandishi wa habari mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia sheria za utoaji wa habari ili kuimarisha mahusiano mazuri baina ya vyombo vya habari na Jeshi la Polisi  katika utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa  ACP Allan Bukumbi katika mdahalo wa Ulinzi na Usalama kwa Wandishi wa Habari ulioratibiwa na Umoja wa Klabu za waandishi wa Habari nchini (UTPC), kupitia Mwamvuli wake wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoani Iringa  (IPC) kuhimiza wandishi kuzingatia maadili wakati wa uandaaji taarifa ili kuondoa mitafaruku kwa jamii.

Kwa upande wake Afisa Msaidizi wa Mafunzo Edmund Kipungu kutoka Umoja wa Klabu za waandishi wa Habari nchini (UTPC) ameeleza kuwa mdahalo huo utasaidia kuondoa changamoto katika vyombo hivyo viwili ambavyo nyakati zingine vimekuwa vikisigana katika kutimiza majukumu yao.

Awali akifungua mdahalo huo Hakimu Mwafong’o ni katibu wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC amesema lengo la mdahalo huo ni kuboresha mahusino  mazuri baina ya jeshi la polisi na waandishi wa habari.

Nao baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wamewashauri wanahabari kuhakikisha wanaandika habari zenye usawa katika pande zote ili kuondoa taharuki katika jamii.

 MWISHO