Nuru FM

Waogeleaji 100 Kuwania Medali,Vikombe Za Klabu Bingwa Tanzania

25 March 2022, 9:16 am

Jumla ya waogeleaji 100 kuanzia Jumamosi Machi 26  watachuana kuwania medali na vikombe  katika mashindano ya klabu bingwa ya mchezo wa kuogelea yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki jijini Dar es Salaam.

Waogeleaji hao wanatoka katika klabu saba ambazo ni Taliss-IST, Dar es Salaam Swimming Club, Bluefins, FK Blue Marlins, Moshi, Morogoro International School (Mis Piranhas) na Mwanza Swimming Club.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Hadija Shebe alisema kuwa mashindano hayo yamepangwa kuanza saa 2.00 asubuhi  na waogeleaji watashindana katika staili tano ambazo ni Freestyle, Breaststroke,Butterfly, Backstroke na Individual Medley.

Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji hao pia watashindana katika relay katika mashindano ambayo yatatumia sheria za Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani (FINA) na pia yatatumika kuchagua timu za Taifa kwa ajili ya kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa duniani.

Alisema kuwa Tanzania inatarajiakushiriki katika mashindano ya Dunia, Jumuiya ya Madola, mashindano ya Afrika kwa waogeleaji wakubwa na vijana.

“Mashindano haya ni makubwa kabisa kwani hata waogeleaji wa Tanzania wanaongelea nje ya nchi wamekuja kushiriki. Ni mashindano pekee ambayo yanatumiwa na TSA kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa.

Tunatarajia kuona ushindania mkali  kwa waogeleaji wetu ili kutafuta nafasi ya kufuzu mashindano ya dunia. Waogeleaji wengi wapo katika maandalizi ya mwisho mwisho kwa ajili ya mashindano hayo, bado tunahitaji wadhamini wa mashindano haya,” alisema Hadija.

Kwa mujibu wa Hadija, kutakuwa na jumla ya vipengele  vya mashindano 100 na kila klabu imetakiwa kuwakilishwa na waogeleaji wawili katika kila kipengele cha mashindano ambavyo pia vimepangwa kutokana na umri katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Pepsi, Azam, Selcom and  Burger 53.